USIANZE DIET YOYOTE KABLA HAUJAFUATA HIZI HATUA 5

1. PATA USHAURI WA DAKTARI.

Mfano wa matatizo ya kiafya yanayosababishwa na uzito uliopitiliza ni kama ugonjwa wa ini unaosababishwa na mafuta yaliyopitiliza, colesterol, pressure ya kupanda, matatizo ya miungio (joints) n.k

Kama umefikia uzito mkubwa wa mwili kuna uwezekano kwamba aidha kuna sababu ya kiafya imechangia kuongezeka kwako uzito au tayari kuna madhara ambayo uzito uliopitiliza umeshafanya kwenye mwili wako.

Ni muhimu kufanya check up ili daktari ahakikishe mwili wako unaweza kustahimili mabadiliko makubwa unayoenda kuyafanya na ndipo akupe ruhusa ya kuanza safari yako ya kupunguza uzito.

Kama tatizo la afya litagundulika aidha utatibiwa kwanza au utashauriwa kuanza taratibu kulingana na uwezo wa mwili wako. Itakuwa vizuri pia ukiendelea kumuona daktari baada ya muda fulani maalumu ili kufuatilia maendeleo yako.

2. CHUKUA VIPIMO VYA MWILI VYA AWALI

Pima uzito na upana wa mwili kabla ya kuanza kupunguza uzito

Pima uzito wako wa mwili na upana wa sehemu mbalimbali kama kifua, kiuno mikono n.k ili ujue mahali unapoanzia.

Hii ni muhimu sana kwasababu ndiyo viashiria vikubwa vya ufanisi wa jitihada zako. Ni rahisi sana kukata tamaa kama hauna kitu kinachokuthibitishia kuwa unapungua.

3. CHUNGUZA CHANZO CHA TATIZO

Kuna sababu nyingi zinazomfanya mtu aongezeke uzito, nyingi zinasababishwa na tabia za ulaji chakula, nyingine sababu ya kutokuwa active/mazoezi na pia kuna magonjwa ambayo yanasababisha kuongezeka uzito kupitiliza mfano PCOS.

Kwa hiyo ni vizuri kama utajichunguza kwanza na ukajua tatizo lako.

Kama tatizo lako ni kuwa na tabia za mbaya za ulaji mfano kupenda kula snacks kama crisps, ubuyu, chocolates, pipi, ice cream, biskuti, keki nk.

Au tabia ya kula usiku sana karibia na wakati wa kulala, au kula chakula kingi sana, take-away kama burgers, chips na pizza. Au tabia ya kunywa vinywaji vyenye calories nyingi kama soda, bia, pombe, energy drinks n.k.

Siku zote ni muhimu kufanyia kazi chanzo cha tatizo kama nia yako ni kuondokana na tatizo hilo milele. Bila kushughulikia chanzo cha wewe kuongezeka uzito wa mwili kupitiliza basi utaendelea kuhangaika na diet na mazoezi maisha yako yote.

Fanya kila uwezalo kujitambua kuwa una tabia hizi na uanze mkakati wa kubadilika ili upate mafanikio makubwa katika kupunguza uzito.

4. KUWA NA MTAZAMO CHANYA

Kabla ya kuanza hakikisha unajiandaa kisaikolojia kwa maana weightloss siyo kitu rahisi. Fahamu kwamba mwili wako umechukua muda mrefu sana kufikia uzito uliofikia leo kwa hiyo upe muda ujirekebishe hadi kupungua kufikia uzito unaoutakiwa.

Kumbuka kila kitu maishani kina kupanda na kushuka kwa hiyo kuwa na mtazamo chanya kutakusaidia kuendelea kupambana hata pale ambapo matokeo yatakuwa taratibu.

Wasio na mtazamo mzuri huwa wanakata tamaa na kurudi kule kule pindi mambo yanapokuwa hayaendi wanavyotaka wao.

5. TAFUTA SUPPORT/PARTNER

Umuhimu wa ushirikiano katika kupunguza unene

 Kuchoka au kukata tamaa huwa  kunatokea unapoanza jitihada za kupunguza uzito wa mwili kwa hiyo ni muhimu kuwa na mtu au kundi la watu ambao mpo kwenye harakati moja ili kupeana moyo na kushauriana.

Partner wako anaweza kuwa rafiki, mwenzi wako ndugu yako au mtu tu uliyefahamiana naye mtandaoni.

Kupunguza mwili na kuishi kwa kufata misingi ya afya ni moja ya maamuzi muhimu katika maisha. Hatua ya kufikia kuamua na kusoma hii post inaonesha upo tayari kwa kufanikiwa.

Ninakukumbusha kufurahia hii safari na kukutakia mafanikio mema!

You may also like...

COMMENT