UKWELI KUHUSU DAWA ZA KUPUNGUZA UZITO AU SLIMMING TEA.

Slimming tea kwa kawaida ni mchanganyiko wa sehemu za mimea mbali mbali ambazo zinaweza kutumika kama majani ya chai.

Kama wewe umekuwa katika safari ya kupunguza uzito kwa muda fulani basi kuna uwezekano mkubwa kwamba umeshakutana na wafanyabiashara wanaouza au wanaotangaza bidhaa za aina hii hasa mtandaoni.

Dawa ya kupunguza uzito

MADAI

Bidhaa hii hutangazwa kwa bidii sana na wauzaji wake kuwa zinapunguza uzito kwa njia kama zifuatazo:

 1. Kupunguza hamu ya kula
 2. Kuyeyusha mafuta mwilini
 3. Kuzuia mafuta kuganda mwilini
 4. Kuondoa sumu mwilini
 5. Kuzuia mafuta yasiingie kwenye mwili (yote yanatoka pamoja na haja kubwa)

UKWELI KWA UFUPI…

 • Ni kweli slimming tea zinasaidia kupunguza uzito wa mwili
 • Ni kweli baadhi ya majani yaliyopo kwenye baadhi ya aina za slimming tea huweza kusaidia kwa namna moja ama nyingine kusaidia kupunguza hamu ya kula.

UKWELI KWA UNDANI…

Hakuna uthibitisho wa kisayansi kupitia tafiti zinazoonesha kuwa slimming tea zinasababisha kupungua uzito kwa muda mrefu.

Kwa lugha rahisi ni kwamba majani haya ya chai husababisha kupungua uzito kwa muda mchache tu na mara nyingi uzito huu hurudi mara tu unapoacha kuyatumia.

Majani ya chai haya ya kupunguza uzito yanasababisha kupungua kutokana na njia moja kuu ambayo ni kuharisha au kupata choo laini hivyo kupelekea mwili kupoteza maji mengi na uchafu uliokuwa kwenye utumbo mpana kutoka.

Hii ni kwasababu karibia slimming tea zote zina kiasi kikubwa sana cha majani yanaojulikana sana duniani kwa jina la SENNA. Mara nyingi kwenye slimming tea, majani haya ndiyo yanakuwa mengi kuliko hata hayo majani mengine yanayosemekana kuleta hizo faida nyingine zinazotajwa kama kuzuia hamu ya kula nk.

Majani ya senna kwa ajili ya kutengeneza dawa za kupunguza unene

Majani ya Senna yanajulikana sana kwasababu yanafanya kazi sawa na kundi la dawa linaloitwa LAXATIVES.

Laxatives ni kundi la dawa zinazosaidia mtu kupata choo kwa urahisi kwa kupitia njia mbali mbali kama kusisimua utumbo mpana kupitisha choo kitoke, kufanya maji yatoke mwilini yaingie kwenye utumbo mpana ili kulainisha choo au nyingine huwa ni mafuta kwa hiyo hufanya uterezi hivyo kusababisha haja itoke kiurahisi n.k

Asilimia kubwa ya watu wanaotumia slimming tea huharisha sana na baada ya muda mfupi hujikuta wamepungua uzito mkubwa ndani ya muda mfupi sana.

Hii ndiyo sababu inayofanya watu wengi wapende kutumia bidhaa hii, kupunguza uzito haraka sana.

MAPUNGUFU…

 1. Uzito unaopungua ni uzito wa maji kupitia kuharisha na si wa mafuta.
 2. Maumivu ya tumbo.
 3. Ni ngumu kujua dozi sahihi ya kutumia au kiasi. Watu wengi wanatumia kiasi kikubwa sana bila kujua.
 4. Huweza kusababisha upungufu wa maji mwilini au dehydration. Hii inaweza kuwa na madhara makubwa sana kutegemea na kiasi cha maji kilichopotea.
 5. Huleta upungufu wa madini ya chumvi mwilini kutokana na maji mengi kutoka mwilini kwa njia ya kuharisha. Hii inaweza kuathiri mapigo ya moyo pamoja na misuli pia.
 6. Utumiaji wa zaidi ya siku 7-12 kunaweza kusababisha utumbo mpana kutoweza kufanya kazi yake pasipokuwepo dawa ya laxative. Hii inafanya ushindwe kupata haja kawaida hivyo kupelekea tatizo la choo ngumu au constipation.

KINACHOTOKEA BAADA YA KUMALIZA KUTUMIA SLIMMING TEA

Kwasababu mwili ulipoteza maji mengi kupitia kuharisha mara tu utakapoacha kutumia dawa hizi za kupunguza uzito mwili wako utafanya juu chini kujirudisha katika hali yake ya zamani.

Utajisikia kunywa vimiminika mara nyingi, na kila utakapokunywa maji mwili wako hautayaachia yapotee kirahisi, utayatunza ili kujazia yalipopungua, pia huweka akiba kama tahadhari ya siku nyingine upungufu huu wa maji utakapotokea.

Kwasababu hii, ni kawaida kwamba utaona uzito ukiongezeka kwenye mzani kila kukicha hadi kufikia uzito ulioanza nao mwanzo.

Wakati mwingine unaweza kupitiliza kabisa!

Kwa ufupi

Slimming tea au dawa za kupunguza uzito sana sana husababisha kupungua uzito wa maji kwa muda mfupi tu kwa njia ya kuharisha. Uzito huu huanza kurudi mara baada ya matumizi kuisha. Kuwa makini kabla ya kutumia, pata ushauri wa daktari, soma maelekezo na usitumie kwa zaidi ya wiki mbili.

Na juu ya yote usisahau kuwa slimming tea zinatumika kama njia za kupunguza uzito haraka ila kwa muda mfupi mfano kama una tukio na unahitaji kupunguza uzito mdogo haraka , au kama tumbo limejaa baada ya kula chakula aina fulani (bloating).

Kwa ajili ya njia za kudumu za kupunguza uzito tafadhali soma makala zifuatazo.

JINSI YA KUPUNGUZA UZITO BILA DIET WALA MAZOEZI

NJIA 3 ZA KUPUNGUZA TUMBO HARAKA!

USIANZE DIET YOYOTE KABLA YA KUFANYA HIZI HATUA 5!

You may also like...

COMMENT