VYAKULA VYA DIET; NJIA 20 ZA KUNUNUA KWA GHARAMA NDOGO

Vyakula vya diet vinasikika sana kuwa na gharama kubwa hivyo kupelekea watu wengi kusita kuanza diet za kupunguza uzito wakihofia kumaliza hela.

Kwanza kabisa maana sahihi ya neno ‘diet‘ ni kila kitu mtu anachokula kwa kawaida mara kwa mara.

Lakini neno hili limebadilishwa maana na kwa muda mrefu sasa linatumika sana kumaanisha vile vyakula mtu anavyokula kwa ajii ya kupunguza uzito au kujenga misuli.

VYAKULA VYA DIET VINA GHARAMA KWELI?

Vyakula vya diet

Ndio na hapana.

Vyakula vingi hata visivyo vya diet ya kupunguza uzito vina gharama ile ile.

Katika makala hii utaenda kuona kuwa sio vyakula vyote vina gharama kubwa, pia utajifunza jinsi ya kupata vyakula hivi kwa bei ndogo kabisa!

1. PIKA CHAKULA MWENYEWE

Siku zote vyakula vya kununua huwa na bei kubwa zaidi. Hii ni kwasababu unaponunua chakula huwa unalipia muda pamoja na nguvu za mpishi.

Wakati mwingine huwa unalipia chombo cha kuhifadhia chakula pamoja na gharama ya kukuletea chakula hicho kama vile unaagiza kutoka mbali.

Ili kuokoa pesa ni vizuri kupika vyakula vya diet yako nyumbani, na vya kununua ukala mara moja moja.

Lakini kama hauna muda kabisa wa kupika basi tafuta sehemu ambayo unaweza kupata vyakula vizuri na vya afya kwa bei rahisi.

2. PANGA VYAKULA VYAKO KABLA YA KUPIKA

Linapokuja suala la kuokoa hela basi kupanga vyakula ndio pointi muhimu zaidi ya zote.

Badala ya kula chakula chochote, chagua siku moja ya wiki upangilie mlo wako wa wiki nzima!

Ukipangilia vyakula kila wiki utajikuta unakula milo sahihi na utaepuka kununua kitu kimoja kimoja.

Pia kupanga chakula kutakusaidia kuokoa muda na kupanga bajeti yako ya maisha kwa usahihi kwasababu utakuwa unafahamu kiasi cha fedha unachotumia kwa ajili ya chakula kila wiki au mwezi.

3.ANDAA ORODHA YA MANUNUZI

Mara baada ya kupanga vyakula vya wiki unatakiwa kuandaa shopping list.

Hii ni orodha ya mahitaji yote ya kuandaa vyakula vyako vya diet kwa ajili ya kupunguza uzito.

Kabla ya kwenda kufanya manunuzi hakikisha una orodha yako kwenye karatasi au simu.

Hii itakusaidia kupunguza gharama ya chakula kwasababu itakuongoza kununua KIASI sahihi.

Pia itakuepusha kununua vitu vingine tofauti ambavyo hauvihitaji ndani ya wiki husika.

4. KAGUA VYAKULA ULIVYONAVYO NYUMBANI

Maandalizi ya vyakula vya diet

Baada ya kuandika orodha ya mahitaji ingia jikoni au stoo ya chakula au kwenye fridge/freezer uangalie vyakula vilivyopo.

Kama ndani bado kuna aina nyingi ya mahitaji ya kupikia basi ni vizuri ukapanga vyakula vya wiki inayofata kuendana na vile ambavyo tayari unavyo nyumbani.

Hii itaepusha uharibifu wa chakula pia utaokoa hela kwa kutonunua kitu tena wakati nyumbani kipo.

Mfano wa mahitaji ambayo huwa yananunuliwa bila mpangilio ni kama mikate, nyanya, vitunguu na mbogamboga nyingine.

Ninaamini hata wewe umewahi kununua nyanya wakati nyumbani zipo na pia umewahi kutupa nyanya nyingi ambazo zilioza kwasababu ulinunua nyingi sana kupita mahitaji.

Ukipanga vyakula vyako wiki nzima kabla, hautakuja kutupa chakula hovyo na utaokoa pesa zako!

5. USITUME MTU SOKONI!

Ubaya wa kutuma mtu kununua mahitaji yako upo kama hivi.

Unayemtuma kama hana ujuzi basi anaweza kuuziwa vitu kwa bei ya juu zaidi au anaweza asiweze kuchagua vyakula vizuri/fresh zaidi.

Na kama unatuma mtu kama dereva piki piki basi hapo ujue kuna uwezekano mkubwa sana wa yeye kupunjwa au kupewa vitu vibaya kuliko vyote hapo gengeni, buchani au sokoni.

Mwisho kabisa unaweza kudhulumiwa hela hata kama ni kidogo.

Unapoenda wewe mwenyewe ambaye unathamini hela yako na chakula chako basi hayo yote utayaepuka!

Watu wengi huwa wanatuma watu sokoni kwasababu wanasema wapo busy wanachoka sana na hawana muda.

Lakini hii ndio sababu ya kuamua kufanya manunuzi ya chakula ndani ya siku moja ambayo upo nyumbani ukiwa uepumzika!

Ukiamua siku moja ya week-end upange vyakula vya wiki nzima, uandae shopping list na uende kununua wala hautatumia muda mrefu!

Ukiweza kufanya hizi utajikuta unaokoa hela nyingi sana na utatamaniungeanza mapema!

BONUS: Kama unaishi na mume/mke hiyo shopping ya wiki/mwezi aidha aende mmoja au wote wawili kwa wakati mmoja na sio kila mtu aende kivyake anunue tu bila kujua nyumbani nini kipo nini hakuna.

Hii hutokea hasa kwenye mikate, baba anarudi nyumbani na mikate mitatu mama anakuja na miwili, baada ya siku 2 mnaongeza tena mnaishia kutupa chakula.

Ni bora list ya mahitaji iwepo, kisha mkusanye hela za kununua vyote kwa wakati mmoja.

6. USIENDE SHOPPING UKIWA NA NJAA

Siku yako ya kufanya manunuzi ya wiki ikifika hakikisha unakula kabla haujatoka nyumbani.

Tafiti zinaonesha kuwa watu wakienda sehemu yenye chakula wakiwa na njaa huishia kununua vitu vingi zaidi hasa vya kula ambavyo hawakutarajia kununua kwasababu ya hamu ya kula! ( 1 )

Utajikuta unanunua soda, juice, keki, sambusa yaani kila kinachotafunika utakitamani tu!

Pia ukiwa na njaa utakuwa unafanya manunuzi kwa haraka ili mradi urudi nyumbani ule.

Ukiwa na haraka hautajipa muda wa kutosha wa kuzunguka na kuchagua mahitaji mazuri na ya bei nzuri.

7. NUNUA KWA WAUZAJI WA NYUMBANI KABLA YA KWENDA SOKONI

Mfano mzuri wa mahitaji ambayo unaweza kuyanunua kwa watu binafsi ni kama mboga za majani, mayai na nyama.

Chunguza kama majirani zako wenye bustani kubwa za mboga wanazo ambazo zipo tayari kununuliwa.

Pia fuatilia wafugaji wa karibu yako, hapo unaweza kupata mayai au unaweza kukuta wamechinja ng’ombe, kuku, mbuzi nk.

Siku zote watu hawa huwa wanauza kwa bei ndogo kwa kiasi kile kile ukilinganisha na wafanyabiashara kwenye soko kubwa.

Au utakuta wanauza bei ile ile lakini wao wanaweka kiasi kikubwa zaidi hasa katika mafungu ya mboga!.

8. LINGANISHA BEI ZA WAUZAJI KABLA YA KUNUNUA

Siku zote katika eneo moja utakuta wauzaji wengi wenye bei tofauti.

Tengeneza mazoea ya kujua sehemu hizi za biashara na bei zao. Hii itakusaidia kuokoa hela hata kama ni kidogo.

Pia jenga mahusiano mazuri na wauzaji ili na wao wapende kukupa bidhaa nzuri na zaidi kama njia ya kukufanya uwe mteja wao wa kudumu!

9. NUNUA BIDHAA ZA BEI NDOGO

Kama unanunua bidhaa zinazotengenezwa na kampuni, hakikisha unalinganisha bei za kampuni tofauti na uchague zenye bei nzuri.

Kwa mfano unahitaji mafuta ya alizeti, chagua yale ya kampuni yenye bei ndogo ili kuokoa hela.

Njia nyingine ya kununua bidhaa za bei ndogo ni kuuliza kama kuna vitu ambavyo vipo kwenye punguzo la bei.

Wauzaji wengi hasa kwenye supermarkets huwa wana bidhaa nyingi sana kwenye SALE. Kwahiyo usiogope kuuliza kama vipo vyakula ambavyo unaweza kupata.

10. USINUNUE MAHITAJI AMBAYO YAMESHAANDALIWA

Vyakula vya kupunguza uzito

Mfano mzuri ni njegere, vitunguu saumu, tui la nazi la kwenye box, na mboga mboga ambazo zimeshakatwa katwa au kusagwa/kutwangwa pamoja na nyama ambazo zimeshakatwakatwa.

Mahitaji yaliyoandaliwa tayari huwa na bei kubwa kulinganisha na yasiyo andaliwa kwasababu unalipia nguvu na muda wa waandaaji.

Kama upo busy sana na hauna muda wa kuandaa mwenyewe basi usihofu, ongeza tu bajeti yako na upate vilivyo tayari.

11. USINUNUE VYAKULA VINGI VILIVYOMO KWENYE VIFUNGASHIO

Mahitaji yaliyopo kwenye vifungashio hasa kwenye supermarkets huwa yana bei kubwa zaidi kuliko yaliyopo wazi.

Mfano ni kama maharage, mchele, pili pili hoho za rangi au bell peppers/capsicum, Karoti, matunda, broccoli, cauliflower nk

Jitahidi kwenda kwenye supermarkets ambazo zina vyakula vilivyo wazi ambavyo unachagua mwenyewe na unapimiwa papo hapo.

Ingawa mara nyingi huwa aina zote zipo, watu wengi sana huwa wanajisahau na wananunua vya kwenye pakti.

Mfano mwingine mzuri ni viungo vya chakula. Ukinunua kwenye pakti au kikopo ujue umetumia gharama kubwa kulingana na ungenunua za kupimiwa papo hapo.

12. NUNUA MBOGA ZA MAJANI NA JAMII YA KUNDE KWA WINGI

Ili kuokoa hela ya chakula ni muhimu kununua vyakula vinavyoshibisha sana huku vikiwa na bei ndogo.

Mfano wa aina hii ya vyakula ni mboga za majani na jamii ya kundekunde mfano maharage, njegere, choroko, mbaazi, njugu nk.

Mboga hizi ni muhimu kujumuishwa kwenye vyakula vya diet za kupunguza uzito kwasababu zina virutubisho vingi, pia zinashibisha sana na zinapatikana kwa bei ndogo.

Watu wengi huwa wanasahau kuwa protini haipatikani kutoka kwenye vyakula vinavyotokana na wanyama tu (mf nyama, samaki, mayai, maziwa, jibini nk)

Mboga jamii ya kunde pia zina kiasi kikubwa sana cha protini hata wanga huku zikiwa zinauzwa kwa bei ndogo sana ukilinganisha na nyama au samaki.

Kwa hiyo hakikisha unapopanga vyakula vyako vya wiki unapanga milo yenye mboga za majani na jamii ya kunde kwa wingi.

13. NUNUA MATUNDA YALIYO KWENYE MSIMU

 Matunda ya kupunguza uzito

Siku zote matunda yanapokuwa katika msimu wake huwa yanauzwa kwa bei ndogo zaidi ukilinganisha na yale yasiyo ya msimu.

Msimu unapoisha yale matunda yanakuwa na bei ghali kwasababu ya upatikanaji wa shida.

Kwa hiyo ukihakikisha unaenda na msimu utafurahia matunda mbalimbali kwa bei nzuri sana!

14. NUNUA AINA YA NYAMA/SAMAKI YENYE BEI NDOGO

Kama unavyofahamu bei ya samaki hutofautiana na aina na kiasi unachohitaji.

Kama unahitaji kutumia gharama ndogo basi jitahidi ujue aina zipi za samaki zina bei ambayo inaendana na bajeti yako.

Katika nyama mfano mzuri ni nyama ya kuku.

Aina na vipande vya kuku hutofautiana bei. Kwa mfano kuku wa kienyeji wana bei kubwa sana kuliko wa kisasa.

Pia sehemu ya kidari ya kuku ina bei kubwa sana ikifuatiwa na sehemu ya juu ya paja(chicken thigh), halafu paja(drumstick) na mwisho vipapatio.

Pia ni muhimu kufahamu kuwa kuku mzima ana bei ndogo kuliko vipande vyake. Kwa hiyo kama una mlo ambao umepanga kula vipande viwili labda, jaribu kununua kuku mzima na inayobaki uweke kwenye freezer au ugawane gharama na mtu wa karibu ambaye anahitaji kuku pia.

15. NUNUA MAHITAJI KWA BEI YA JUMLA au NUNUA KIASI KINGI

Vyakula vya diet ya siku 3

Kama una chochote ambacho unaweza kununua kingi kwa bei ya jumla jitahidi kufanya hivyo na kisha kuhifadhi kinachobaki kwenye freezer.

Mfano wa mahitaji ambayo unaweza kununua kwa bei ya jumla ni mayai, chumvi, tui za nazi za kopo nk.

Pia unaweza kununua kindoo cha nyanya, vitunguu, viazi nk badala ya kununua kwa mafungu.

Ukifata ushauri huu utajikuta gharama yako ya chakula inapungua sana.

Kama unaona hautaweza kuvihifadhi kwa muda mrefu basi unaweza kununua pamoja na mtu mwingine aliye jirani halafu baadaye mgawane sawa kwa sawa.

16. EPUKA KUNUNUA SNACKS NA JUNK FOODS

Snacks na junk foods kama soda, biskuti, keki, chocolates, crisps,visheti nk vikiendekezwa huwa vinapelekea kutumia hela hovyo.

Kama upo kwenye mkakati wa kupunguza uzito na kuishi healthy basi jitahidi uhakikishe umenunua vyakula vyako vyote vya afya.

Hakikisha unanunua snacks ambazo zinaendana na vyakula vya diet unayoifatilia.

17. USITUPE CHAKULA!

Aina ya mahitahi/vyakula vinavyoongoza kwa kutupwa ni kiporo, mikate pamoja na mboga mboga zote zinazoharibika haraka kama nyanya, karoti, matango nk.

Ukishanunua mahitaji yako ya wiki nzima hakikisha unatumia kila kitu. Kama kuna chochote kilichobaki hakikisha unakihifadhi kwenye fridge/freezer.

Hii inajumuisha pia chakula ambacho umeshindwa kumaliza kutokana na sababu moja au nyingine.

Watu wengi sana wanapoteza hela nyingi kila siku kwa kutupa chakula. Hii ni kwasababu hawapangilii vyakula na wananunua vitu vingi kuliko mahitaji.

Ukifata tips zote katika makala hii basi utajikuta ukipunguza sana tabia ya kutupa vyakula.

Kama unaishi na familia yako basi wahimize kupakua kile tu wanachohitaji. Mwishoni atakayeshindwa kumaliza aweke kwenye kicontainer chake na ahifadhi kwenye fridge ale baadaye au hata kesho yake.

18. NENDA SOKONI MARA CHACHE KWA WIKI

Tafiti nyingi zimeonesha kuwa watu wanaoenda sehemu ya mauzo mara nyingi huwa wanatumia hela nyingi zaidi kuliko wale wasioenda mara kwa mara.

Hii ni kwasababu kila ukienda lazima utakuta vishawishi vya kununua hata vitu ambavyo hauvihitaji!

Jaribu kwenda sokoni ile mara moja kwa wiki kununua kila kitu. Na ukienda siku nyingine labda kufata mboga za majani tu!

Ukifanya hivi utaokoa hela nyingi sana kwasababu hautanunua vitu bila kupanga.

19. PANDA BUSTANI YA MBOGA

Vyakula sahihi vya kupunguza unene

Kama vile una nafasi kwenye makazi yako unaweza kupanda mboga mboga kama za majani, nyanya, vitunguu, bilinganya nk.

Mara nyingi hii haiitaji kazi kubwa sana hasa kama ni kwa ajili ya familia tu. Ukifanya hivi utaweza kuokoa hela nyingi kwasababu mboga mboga hizi huwa zinaliwa kila siku

20. PUNGUZA GHARAMA YA STAREHE NYINGINE

Wapo watu ambao hulalamika kuwa hawawezi kula kwa afya sababu ya gharama huku kila week-end wanatoka, wanakunywa sana, wanavaa vizuri sana, wanabadili mtindo wa nywele kila wiki na mengine mengi.

Hakuna kitu muhimu katika maisha kama afya, na afya inapatikana jikoni kwanza.

Kama hauwezi kuwekeza kidogo kwenye kula kwa afya upunguze uzito ukawa fit basi utakuja kutumia hela nyingi sana hapo baadaye kurudisha mwili wako kwenye hali nzuri.

Ubaya ni kwamba hatujui lini miili yetu itashindwa kubeba mafuta tunayojizazia kwa kula vibaya.

Mwingine pressure, kisukari, ini, moyo, figo vinaanza kufeli akiwa na miaka 25, mwingine 30, mwingine 35 hatujui lini.

Huwa inaanza ghafla tu tunajikuta kila mwezi kwenye hospitali tukinunua dawa na kufanya mara vipimo vyenye gharama za ajabu hadi tunajuta

Tujitahidi kuweka bajeti ya vyakula vya afya kuwa juu ya starehe.

Ninatumaini umejifunza kitu kipya katika makala hii ambacho kitaenda kukusaidia kuokoa fedha nyingi katika bajeti yako ya vyakula vya diet.

Usisahau kuacha comment yako kwa maswali au nyongeza yoyote.

SOMA: DIET YA KABICHI YA KUPUNGUZA UZITO WAKATI WA DHARURA

SOMA: MAZOEZI YA KUPUNGUZA UNENE WA MIKONO

SOMA: VIFUNGUA KINYWA HIVI VINAVYOSAIDIA KUPUNGUZA UZITO

You may also like...

COMMENT