JINSI YA KUPUNGUZA UZITO KWA WANAFUNZI WA CHUO.

Kundi la watu ambao hupata changamoto zaidi katika kupunguza uzito ni wanafunzi wanaoishi kwenye hostel.

Vyuo vingi haviruhusu wanafunzi kupika vyakula vyao hivyo kusababisha wengi wao kuishia kutegemea kununua vyakula ambavyo mara nyingi haviendani na misingi ya afya ya lishe.

Wakati ninasoma chuo niliongezeka zaidi ya kilo 15 ndani ya miaka mitatu na pia niliweza kupunguza zaidi ya kilo 15 ndani ya muda mfupi zaidi kwa hiyo ninadhani ninaweza kuchangia kuhusu changamoto hii.

Kabla ya kuanza kukuambia jinsi ya kupunguza uzito wako na kuanza kuishi maisha ya afya ukiwa chuo, ngoja nikuoneshe sababu kuu zinazofanya wanafunzi wengi kuongezeka uzito au kushindwa kupunguza uzito wakiwa wanasoma.

1. FAST FOODS

vyakula vinavyoongeza uzito

Mfano mkuu wa fast foods inayochangia zaidi kuongeza uzito ni chips. Mara nyingi wanafunzi huwa na haraka na chips ni chakula kinachopatikana kwa wingi sana ndani ya muda mchache.

Chips husababisha kuongezeka uzito kwasababu viazi ni chakula cha wanga na kama umesoma makala nyingine yoyote kwenye blog hii utakuwa unajua kwamba vyakula vya wanga ndivyo vinavyoongoza katika kusababisha ongezeko la uzito.

Pia chips hupikwa na mafuta mengi sana kwa hiyo ndani ya mlo mmoja mara nyingi unaweza kukuta mtu amekula kiasi cha calories cha siku nzima.

2. SNACKS/VYAKULA VYEPESI

vyakula vya kuepuka ili kupunguza uzito

Hizi ni kama Chocolate, biskuti, cookies, crisps za viazi/ndizi/mihogo, ice creams, maandazi, keki, kachori, sambusa, vitumbua, chapati nk

Ubaya wa snacks ni kwamba:

  • KWANZA: mara nyingi huundwa na kundi moja tu kuu la chakula ambalo ni wanga.
  • PILI: huwa na sukari nyingi sana.
  • TATU: huwa na ukubwa mdogo hivyo kukufanya ule vingi bila kujisikia kushiba sana.

Kutokana na kiasi kikubwa sana cha wanga hasa sukari, mara nyingi snacks husababisha mtu atengeneze addiction kama watu wanavyokuwa addicted na vilevi kama pombe, sigara au madawa ya kulevya.

Snacks pia huwa zinapatikana sehemu nnyingi, ndani ya muda wowote na kwa bei ndogo hivyo kuzifanya chakula kinachopendwa sana na wanafunzi ambao huwa mara nyingi huwa ni watu wenye haraka na wasiokuwa na kiasi kikubwa cha fedha.

3. VINYWAJI VYENYE SUKARI

Epuka vinywaji hivi ili kupunguza uzito

Nadhani unaweza kukubaliana na mimi kuwa wanafunzi wengi hupendelea kunywa soda au juice kuliko hata maji.

Hii ni sababu ya kiasi kikubwa cha sukari kilichopo kwenye vinywaji hivi.

Tukiachana na utamu, mara nyingi wanafunzi huvinywa kwasababu sukari hufanya mtu apate nguvu ya haraka.

Kwasababu wanafunzi hutumia nguvu nyingi sana katika kusoma mara nyingi bila wao kujijua hujikuta wanakunywa vinywaji vingi vya sukari ili kupata ile nguvu ya kuchangamka na kutilia maanani masomo.

4. STRESS

Jinsi stress/mawazo husababisha kuongezeka uzito

Watu wengi hufikiri kuwa stress kiujumla humfanya mtu apungue uzito. Hii ni kweli lakini huwa inasahaulika kwamba kuna stress za aina kuu mbili ambazo ni stress za muda mfupi na za muda mrefu.

Stress za muda mfupi ni zile kama za mitihani, utagundua kuwa wanafunzi wengi wanaweza kupunguza uzito kipindi cha mitihani kwasababu mbali mbali kama kushindwa kula kutokana na hofu ya kutomaliza kusoma kila kitu.

Stress za muda mrefu ni zile zinazoendelea bila kukoma mfano kozi zenye masomo magumu sana, kufeli mitihani mara kwa mara, kutofurahia masomo, hofu ya wazazi, hofu ya walimu, matatizo katika mahusiano ya kimapenzi n.k

Stress za muda mrefu hufanya mwili wako utengene hormone inayoitwa cortisol ambayo mwisho wa siku hukufanya ule sana hasa vyakula vyenye sukari au mafuta kiasi kikubwa.

Stress ya aina hii huishia kufanya mtu atumie chakula kama chanzo cha kujiliwaza hivyo kusababisha ulaji uliopitiliza na kuongezeka kwa uzito.

Baada ya kukuelekeza sababu zinazosababisha wanafunzi wengi kushindwa kupunguza uzito nitakueleza njia 5 ambazo ukizifata bila shaka utaanza kuona uzito wako ukipungua bila vikwazo!

1. KUNYWA MAJI MENGI

Mamia ya tafiti za kisayansi yanaonesha kuwa kuongeza kiasi cha maji tunayokunywa kwa siku husaidia sana katika kupunguza uzito.

Hii ni kwasababu maji huchukua nafasi kubwa tumboni hivyo kukufanya ujisikie umeshiba mara moja!.

Pia maji husababisha balance ya hormone inayotupa hisia ya kushiba na ya hamu ya kula hivyo kutuepusha kusikia njaa mara kwa mara.

Ili kukusaidia kupunguza uzito, kunywa maji mengi kwa siku hasa hakikisha unakunywa angalau NUSU LITA ya maji kabla ya kila mlo.

Ina maana ukishapakua chakula chako kabla haujaanza kula kunywa maji ndipo ule.

Hii itakufanya uishie kula kiasi kidogo cha chakula hivyo kukusaidia kupunguza uzito.

2. PUNGUZA KIASI CHA CHAKULA

Kuongezeka uzito au kushindwa kupunguza uzito ni kiashiria kwamba unakula chakula kingi kupita mahitaji ya mwili wako.

Kwa hiyo ili kupungua lazima upunguze kiasi cha chakula. Kama ulikuwa unakunywa chai na chapati mbili basi kula moja. Kama ulikuwa unakunywa soda mbili kwa siku basi kunywa moja kama ulikuwa unajaza sahani pakua nusu.

Hii ni hatua rahisi ambayo kila mtu anaweza kuifata na itakusaidia kupunguza uzito na pia kuokoa pesa.

3. ONGEZA VYAKULA VYA PROTINI

Fungu hili la chakula ndilo linaloongoza katiba kusaidia kupunguza uzito na kufanya mwili wako uwe wa afya!

Hii ni kwasababu protini huchukua muda mrefu sana kumeng’enywa tumboni hivyo hukaaa humo kwa muda mrefu na kutufanya tusikie tumeshiba sana.

Protini pia ndiyo malighafi kuu katika utengenezwaji wa misuli ambayo ndiyo nyenzo kuu ya uyeyushwaji wa mafuta mwilini.

Wanafunzi wengi hula kiasi kidogo cha vyakula vya protini kwasababu kwa kawaida vyakula hivi huwa na gharama kubwa kuliko vyakula vya wanga kama chips.

Lakini ninaamini kuwa ukipanga bajeti yako vizuri unaweza kupata nafasi ya kuongeza fungu hili la chakula kwenye diet yako bila tatizo lolote!.

Anza na mayai mawili hasa ya kuchemsha asubuhi badala ya chai na mikate/maandazi/chapati/vitumbua/mihogo/viazi nk

Au unaweza kula supu/mchemsho wa nyama bila kuongeza wanga kama chapati au ndizi.

Zipo tafiti zinazoonesha kuwa watu wanaokula kifungua kinywa chenye kiasi kikubwa cha protini hasa mayai hupungua uzito zaidi na hubakia kwenye uzito wa wa afya kwa muda mrefu ukilinganisha na wanaokula wanga mwingi.

4. KULA SALAD MBICHI

Kama hostel kwenu hamruhusiwi kupika bado unaweza kupunguza kiasi kikubwa cha uzito wako kwa kujiandalia salad mbichi.

Nunua matango, nyanya, vitunguu, pilipili hoho, karoti, kabichi na matunda yasiyo na sukari nyingi sana mfano maparachichi , zabibu, peaches (mafyulis) na berries.

Katakata na utengeneze salad tamu ambazo unaweza kula zenyewe au pamoja na nyama, samaki au mayai ambayo utanunua kutoka canteen.

Vyakula vibichi husaidia sana kupunguza uzito kwasababu huwa na kiasi kikubwa sana cha nyuzi nyuzi au fibre.

Kwasabababu hii mwili huhitaji muda mwingi zaidi kuvimeng’enya hivyo hukufanya ushibe haraka na ujisikie umeshiba kwa muda mrefu zaidi.

Pia vyakula hivi huwa na kiasi kidogo cha calories kwasababu havijaongezewa calories nyingine ambazo huwa tunaongeza wakati wa upishi kama mafuta.

Hivyo unaweza kula salad kiasi kikubwa na kushiba bila kuwa kuingiza calories nyingi mwilini.

5. FANYA MAZOEZI YA VIUNGO

mazoezi ya kukimbia kwa ajili ya kupunguza unene

Lengo kuu la kufanya mazoezi ni kuulazimu mwili wako kutumia kile chakula ulichokula kutengeneza nguvu badala ya kuacha kiende kubadilishwa kuwa mafuta na kuhifadhiwa mwilini.

Kama umekula kiasi kidogo cha chakula kwa siku, mazoezi husaidia kuongeza bidii ya mwili kuyeyusha mafuta yako kugeuza nguvu hivyo kukusababisha upunguza uzito.

Mazoezi ni kichocheo cha utengenezaji wa misuli mwilini, na kama ulivyokwisha ona mapema kwenye makala hii, misuli ndiyo nyenzo kuu ya kuyeyusha mafuta.

Kwa hiyo unavyozidi kufanya mazoezi ndivyo unavyozidi kujenga misuli na ndivyo unavyofanya mwili wako uwe sanifu zaidi kuyeyusha mafuta na kukusaidia kupunguza uzito.

Ni muhimu sana kutengeneza muda na tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara.

Tambua kwamba siyo lazima uende gym ili kupunguza uzito, unaweza kupata mafanikio makubwa kwa kufanya mazoezi mwenyewe ukiwa campus kwenu.

Kwa mfano unaweza kuanza kukimbia kwenye uwanja wenu wa michezo au kujiunga kwenye timu ya michezo ya darasa.

Kama unapata hofu au haupendelei kufanya mazoezi mbele ya watu basi unaweza kuamka asubuhi sana na kukimbia angalau kwa nusu saa kabla ya watu hawaajamka kisha kuendelea na ratiba zako nyingine.

Unaweza kupunguza uzito ukiwa sehemu yoyote ile cha muhimu ni kuamua na kuwa tayari kufanya mabadiliko.

Hakikisha unapata usingizi wa kutosha kwa kupunguza shughuli nyingine zisizokuwa za maendeleo kwako kwa mfano kuangalia series masaa mengi.

Pia tafuta njia ya kutatua matatizo pamoja na stress kama kuongea na mshauri wa wanafunzi n.k

Wazo mojawapo zuri ni kutafuta wenzako ambao aidha wanahitaji kupunguza uzito kama wewe au wanapenda tu maisha ya afya na kufanya mazoezi.

Jiungeni pamoja kivyenu au anzisheni club ya mazoezi na muhakikishe mnashirikiana na kujifunza pamoja jinsi ya kuishi maisha kwa kufata misingi ya lishe sahihi pamoja na mazoezi.

Ninatumaini umeweza kupata mawazo mazuri ambayo yatakusaidia kupunguza uzito ukiwa chuoni.

Tafadhali washirikishe makala hii na wenzako na comments niambie kama utafata ushauri huu na kuanza safari yako ya kupunguza uzito.

Pia unaweza kuniambia changamoto zako za kupunguza uzito ukiwa chuoni au tushirikishe ushauri zaidi wa jinsi ya kupunguza uzito ili wanafunzi wengine waweze kujifunza zaidi!

Ninakutaka mafanikio mema!

You may also like...

COMMENT