DIET YA MTINDI: PUNGUZA KILO 3-5 KWA SIKU 7

Diet ya mtindi ni mojawapo ya diet fupi ambayo inafahamika na kufuatwa na watu wengi sana.

Katika makala hii utaona faida za maziwa ya mtindi kwa afya pamoja na jinsi ya kutumia maziwa haya kwa ajili ya kupunguza uzito wako kwa muda mfupi tu.

Diet hii hutumika kama hatua ya dharura ya kupunguza uzito ndani ya muda mfupi kwa hiyo hautakiwi kuifata kwa zaidi ya siku 7.

Hii ni diet ya 3 ya dharura kuandikwa kwa undani katika blog hii. Kama ulikosa hizo makala nyingine unaweza kuzisoma hapa ili kulinganisha diet hizi na kuona ipi itakufaa zaidi kutokana na malengo yako!.

SOMA: DIET YA SUPU YA KABICHI

SOMA: DIET YA JUISI YA UKWAJU

SOMA: DIET YA MAYAI

Yaliyomo:

 • Kiasi cha Kalori kwenye mtindi
 • Faida 10 za maziwa ya mtindi
 • Jinsi ya kuanza diet ya mtindi
 • Vyakula vinavyoruhusiwa kwenye diet hii
 • Ratiba ya vyakula ya siku 7
 • Tahadhari

KIASI CHA VIRUTUBISHO KWENYE MTINDI

Kwenye 100g au 100 ml za mtindi usiopunguzwa mafuta kuna…

VIRUTUBISHO KIASI
Kalori 61 Cal
Protini 3.5 g
Wanga (Sukari) 4.7 g
Mafuta 3.3 g
Nyuzi nyuzi 0 g
Maji 88%

Ina maana ili kujua kiasi cha kalori kwenye nusu lita ya mtindi ambayo ni sawa sawa na gramu 500 itabidi uzidishe 61 X 5 = 305 Cal

FAIDA 10 ZA MAZIWA YA MTINDI

1. KUIMARISHA AFYA YA MFUMO WA MMENG’ENYO WA CHAKULA

Maziwa ya mtindi hutengenezwa kwa kuchachisha maziwa. Hatua hii hutokea pale ambapo aina fulani ya bacteria hubadilisha sukari ya kwenye maziwa (Lactose) kuwa asidi ya Lactic (Lactic acid).

Asidi hii ndiyo huleta ladha ya uchungu na muonekano wa kuganda kwa maziwa.

Bacteria hawa waliopo kwenye maziwa ya mtindi ni muhimu sana katika kuimarisha bacteria salama waliopo kwenye utumbo wa binadamu.

Kutokana na hili, maziwa ya mtindi husaidia sana katika matatizo kama kuharisha, choo ngumu(constipation), inflammation ya utumbo, pamoja na allergy ya maziwa(Lactose intolerance)

2.KUIMARISHA KINGA YA MWILI

Baadhi ya bacteria salama wanaotengeneza mtindi wana uwezo wa kusisimua mfumo ya kinga mwilini kutengeneza seli aina ya T-cells ambazo ni muhimu sana katika kupambana na magonjwa.

Kutokana na hili, tafiti huonesha kuwa watu wanaotumia mtindi mara kwa mara huwa na wanapata kinga nzuri zaidi dhidi ya maambukizi hasa ya magonjwa ya tumbo na za njia ya hewa kama mafua.

3.AFYA YA MFUMO WA UZAZI

Maziwa ya mtindi yameonekana kisayansi kuhusika katika kukinga wanawake dhidi ya maambukizi ya fungus wa sehemu za siri( Candidal Vaginitis) pamoja na maambukizi ya bacteria (Bacterial vaginosis).

Hii ni kwasababu bacretia salama waliopo kwenye maziwa ya mtindi husaidia ku-balance Ph ya mwili kitu ambacho kinafanya bacteria na fungus aina hii (Candida) wasiweze kuishi kwenye sehemu hiyo ya mwili.

4. VITAMIN NA MADINI

Maziwa ya mtindi yana vitamin muhimu sana kwa afya ya binadamu kama

 • Vitamin A
 • Vitamin B (B1, B2, B3, B6, B9, B12)
 • Vitamin E
 • Calcium
 • Phosphorus

5. CHANZO CHA PROTINI

Kama ambavyo imetajwa mara nyingi sana katika makala mbali mbali kwenye blog hii, Protini ndilo fungu kuu la chakula katika kusaidia kupunguza uzito.

Maziwa ya mtindi yana kiasi kikubwa cha protini. ( 1 )

Zipo aina kuu 2 za protini kwenye mtindi nazo ni Casein 80% na Whey 20%

Protini ya Casein husababisha madini kama Calcium na phosphorus yaweze kupita kutoka tumboni kuingia kwenye mzunguko wa damu, hivyo kusaidia shughuli mbali mbali zinazotegemea madini haya kwa mfano utengenezaji na uimarishaji mifupa. ( 2 )

Pia casein husaidia sana katika kupunguza presha ya damu hasa kwa watu wenye tatizo la presha ya kupanda. ( 3 , 4 )

Protini ya whey ndiyo inayofahamika sana katika kupunguza uzito na kujenga misuli hasa kwa wanaonyua vyuma.

Hii ni kwasababu protini ya whey ndiyo inayotumika kutengeneza unga wa protini (Protein powder) ambao unatumiwa sana na wanamazoezi.

Hii pia husaidia katika kupunguza uzito na kushusha presha ikae sawa kwa watu wenye tatizo la presha ya kupanda.( 5 , 6 )

SOMA ZAIDI: NIA 10 ZA KUPUNGUZA UZITO BILA DIET WALA MAZOEZI

6. KUIMARISHA MIFUPA

Maziwa ya mtindi yana kiasi kikubwa cha madini ya calcium ambayo ni muhimu sana katika kujenga mifupa.

Kula mtindi kwa kawaida huweza kusaidia kukulinda dhidi ya tatizo la mifupa kupata ufa au kuvunjika kirahisi hasa kwa watu wenye umri mkubwa(Osteoporosis)

Kutokana na tafiti mbalimbali za kisayansi, kunywa maziwa kumeonekana kupelekea mtu kuwa na mifupa migumu na yenye afya.( 7 , 8 )

7. KINGA DHIDI YA CANCER

Ukilinganisha na maziwa fresh, maziwa ya mtindi yana kiasi kikubwa zaidi cha asidi aina ya Conjugated linoleic acid.

Asidi hii imeripotiwa kuweza kusisimua mfumo wa kinga ya mwili kupigana na maambukizi mwilini.

Pia inafahamika kusaidia mwili kuua seli za cancer au kuzifanya zisiendelee kukua.

8. KUZUIA PRESSURE YA KUPANDA

Tatizo la pressure ya kupanda ni moja ya chanzo kikubwa cha magonjwa ya moyo duniani.

Tafiti zinaonesha kuwa kuna uhusiano kati ya kunywa mtindi na maziwa kwa ujumla na kupunguza pressure ya damu.

Hii ni kwasababu maziwa haya yana madini ya Potassium ambayo hufanya mwili uondoe madini ya Sodium hivyo kusabababisha pressure ya damu ishuke kwa wale ambao huwa inapanda.

Madini ya Sodium yanapatikana hasa kwenye chumvi. Yanapokuwa kwa wingi kwenye damu husababisha pressure kupanda.

Kwasababu hii, watu wenye tatizo la pressure ya kupanda hushauriwa kuepuka vyakula vyenye chumvi.

Pia madini ya Calcium, Potassium na Magnesium kwenye maziwa ya mtindi husaidia kupunguza uwezekano wa mtu kupata kiharusi (Stroke) tatizo ambalo huweza kusababishwa na pressure kubwa sana ya damu.

Kwa hiyo kunywa maziwa ya mtindi mara kwa mara kunaweza kupunguza pressure kwa watu ambao tayari pressure yao ipo juu ( 9 )

Kiasi kilichoonekana kuleta faida hii ni kuanzia ml 438 – ml 657 au kwa wastani wa nusu lita kwa siku.

9. KUZUIA KISUKARI TYPE 2

Zipo tafiti za kisayansi zinazoonesha kuwepo uhusiano kati ya maziwa ya mtindi na kuzuia tatizo la kisukari ( 10 )

Tafiti nyingine imeonesha kuwa maziwa ya mtindi yanahusika katika kuzuia tatizo la kisukari type 2 kwasababu wale bacteria wazuri wanaotumika kugandisha maziwa husaidia kushusha sukari mwilini. ( 11 )

10. KUPUNGUZA UZITO

jinsi ya kupunguza uzito kwa kufata diet ya mtindi

Kwanza kabisa maziwa ya mtindi husaidia kupunguza uzito kwasababu yana kiasi kikubwa cha protini.

Na kama ilivyoongelewa katika makala nyingi sana kwenye blog hii, vyakula vya protini vinaongoza katika kusaidia kupunguza uzito kwasababu

 • Mwili huhitaji muda mrefu zaidi kumeng’enya vyakula vya protini hivyo ukila utahisi kushiba kwa muda mrefu na itakuzuia kula kula kila wakati.
 • Mwili hutumia nguvu nyingi zaidi katika kumeng’enya vyakula vya protini kuliko kundi lingine la vyakula.
 • Protini ndiyo malighafi kuu ya kutengeneza misuli mwilini. Na misuli ni nyenzo muhimu sana katika kusaidia uyeyushaji wa mafuta. Pia unapokuwa na kiasi kikubwa cha misuli unaweza kufanya shughuli/mazoezi kwa bidii zaidi hivyo kuyeyusha mafuta kwa ufanisi zaidi.

Ukiachia mbali protini, aina nyingine ya kirutubisho kinachosaidia kupunguza uzito ni madini ya Calcium.

Tafiti zinaonesha kuwa madini ya calcium yanaweza kupelekea ufanisi zaidi katika kupunguza mafuta mwilini hasa kwenye tumbo.

Katika tafiti mojawapo watu waliokuwa wanatumia maziwa ya mtindi walionekana kupungua uzito 22% zaidi ya wasiokula mtindi.

Pia watu hawa waliondoa mafuta mwilini mwao 62% zaidi ya ambao walikuwa hawatumii maziwa ya mtindi.

Zaidi ya hapo wale waliokuwa wanakunywa mtindi 81% ya mafuta waliyoyaondoa mwilini yalitoka kwenye eneo la tumboni.

Kwa hiyo kama unahitaji kupunguza uzito hasa ukubwa wa tumbo ni muhimu kuanza kunywa kiasi sahihi cha maziwa ya mtindi.

JINSI YA KUFATA DIET YA MTINDI KWA AJILI YA KUPUNGUZA UZITO

Kwanza kabisa diet hii inatakiwa kufatwa kwa siku 3-7 tu na si zaidi.

Hii ni kwasababu diet hii ni ya dharura kwa hiyo inalenga kukufanya ule kiasi kidogo cha chakula ili kupunguza uzito haraka.

Ni vizuri kuanza kuifata kwa siku 3 na kuangalia mwili wako unavyojisikia.

Kama utaweza kuendelea basi malizia hadi siku 7 lakini kama utashindwa unaweza kuishia hapo.

VYAKULA VINAVYORUHUSIWA

Diet ya siku 7 kwa ajili ya kupunguza tumbo
 • Maziwa ya mtindi yaliyopunguzwa mafuta(Low fat yogurt)
 • Matunda mf Apples, ndizi, mapeasi, berries
 • Mbegu za chia
 • Mkate wa brown (brown bread)
 • Viazi na ndizi mbichi
 • Nyama na samaki
 • Kachumbari au salad (nyanya, matango, karoti, vitunguu nk)
 • Kabichi
 • Mayai
 • Karanga
 • Chai

KWANZA: Hakikisha unaongeza kijiko kidogo kimoja cha mbegu za chia katika maziwa ya mtindi na kuloweka kwa dakika 5 kabla ya kula.

Mbegu za chia zinasaidia sana katika kupunguza uzito kwasababu zina kiasi kikubwa sana cha protini.

PILI: Wali wa brown utaongeza jitihada za kupunguza uzito kuliko wali mweupe.

Ukila wa brown utajisikia umeshiba hara na kwa muda mrefu zaidi hivyo kukuzuia kula sana.

Wali ambao utakufanya upunguze uzito zaidi ya wote ni wali wa cauliflower!

Una kiasi kidogo sana cha wanga na unaweza kula zaidi ya kipimo kilichotajwa kwenye diet hii.

TATU: Epuka kutumia sukari nyingi au asali nyingi. Sukari hufanya mwili uache kuyeyusha mafuta kwasababu inapoingia kwenye mwili huifanya ile hormone inayoyeyusha mafuta ipungue sana au itoweke.

Ukitumia mbadala wa sukari (sweetners) utapungua kiasi kikubwa zaidi. Asali isizidi kijiko kidogo kimoja.

Kama hauna mbadala wa sukari unaweza kutotumia sukari kabisa. Lakini kama hauwezi kujizuia basi jitahidi sana kuweka sukari kwa mbali.

Kutotumia sukari au asali kabisa kutaleta matokeo makubwa zaidi.

NNE: Epuka kutumia mafuta mengi kwenye kupika mboga mboga. Kijiko kidogo kimoja kinatosha kuungia mboga.

Pia unapopika nyama na samaki hakikisha unachemsha na unakula minofu (Steak) badala ya vipande vyenye mafuta.

TANO: Ni muhimu kufahamu na kutumia vipimo maalumu vya chakula.

Utakapoona kipimo kama “Wali kikombe kimoja” au “wali vijiko vikubwa 16” kumbuka hivi si vikombe tunavyonywea chai.

Bali vipo vikombe maalumu kwa ajili ya kupimia chakula kama unavyoona hapa chini.

Kama hauna vipimio hivi basi tumia vijiko vikubwa. Baadaye unaweza kununua vipimo hivi kwa bei rahisi tu ili ikusaidie huko mbeleni.

RATIBA YA CHAKULA YA DIET YA MTINDI

SIKU YA 1 + 2

ASUBUHI

 • 1/4 L mtindi low fat
 • Mbegu za Chia kijiko kidogo 1
 • 1/4 Apple

MCHANA

 • 1/4 L mtindi low fat
 • Mbegu za Chia kijiko kidogo 1
 • Kikombe kimoja cha wali uliopikwa = vijiko vya chakula 16
 • Mboga za majani

USIKU

 • 1/2 L mtindi
 • Mbegu za Chia kijiko kidogo 1
 • 1/4 Apple
 • Karanga/almonds Vijiko vikubwa 2

SIKU YA 3+4

ASUBUHI

 • 1/4 L mtindi
 • Mbegu za Chia kijiko kidogo 1
 • Mkate wa brown slesi 1

MCHANA

 • 1/4 L mtindi
 • Mbegu za chia kijiko kidogo 1
 • Kiazi cha kuchemsha 1
 • Vipande vya nyama/kuku vya kuchemsha
 • Kachumbari/salad

USIKU

 • 1/2 L mtindi
 • Mbegu za Chia kijiko kidogo 1
 • Tango 1

SIKU 5+6

ASUBUHI

 • 1/4 L mtindi
 • Mbegu za Chia kijiko kidogo 1
 • 1/2 ndizi mbivu

MCHANA

 • 1/4 L mtindi
 • Mbegu za Chia kijiko kidogo 1
 • Samaki wa kuchemsha
 • Ndizi mbichi 1
 • Salad (Tango 1, nyanya 2, kitunguu)

USIKU

 • 1/2 L mtindi
 • Mayai 2 ya kuchemsha
 • Salad

SIKU YA 7

ASUBUHI

 • 1/4 L mtindi
 • Mbegu za Chia kijiko kidogo 1
 • 1/4 Apple

MCHANA

 • 1/4 L mtindi
 • Mbegu za Chia kijiko kidogo 1
 • Wali kikombe 1 = Vijiko vikubwa 16
 • Vipande vya nyama
 • Tango 1

USIKU

 • 1/2 L mtindi
 • Mbegu za Chia kijiko kidogo 1
 • Samaki
 • Salad (Tango 1, Nyanya 2 , Kabichi)

TAHADHARI

Diet ya mtindi ni nzuri kwa kupunguza kiasi kikubwa cha uzito kama hatua ya dharura tu.

Haupaswi kuifata diet hii zaidi ya wiki moja kwasababu mwili wako unahitaji virutubisho vya aina nyingine.

Watu wasioruhusiwa kufata diet hii ni wale wenye

 • Ujauzito
 • Matatizo ya figo hasa Kidney stones (mawe kwenye figo)
 • Matatizo ya ini
 • Tatizo la cholesterol nyingi

Hii ni kwasababu wanawake wajawazito wanahitaji lishe kamili yenye virutubisho kutoka kwenye vyakula mbalimbali.

Maziwa ya mtindi yana kiasi kikubwa cha calcium ambayo inaweza kuongeza tatizo la mawe ya kwenye figo.

Pia maziwa ya mtindi yana mafuta hivyo kuweza kuchangia tatizo la Cholesterol kwa wale ambao tayari linawasumbua sana.

KWA UFUPI

Diet ya mtindi ni nzuri sana kwa kupunguza uzito mkubwa ndani ya muda mchache.

Hakikisha unaendelea kula lishe sahihi ili uendelee kupunguza uzito baada ya kumal1iza kufatilia diet hii.

Niambie kwenye sehemu ya comments kama umewahi kufanya diet ya mtindi au kama ungependa kuanza.

Pia ukiifata diet hii tafadhali nishirikishe matokeo yako kupitia hii blog au instagram na facebook @gigimaenda

Jiandikishe ufollow blog hii ili usikose makala ijayo ya diet ya mayai kwa ajili ya kupunguza uzito haraka!


You may also like...

4 Responses

 1. Magreth says:

  Hi, me ndiyo naanza kesho.. nina kg 91.. so will see and I will bring feedback.

 2. Daniel says:

  mi niña cholesterol na mtindi nliona ulinisaidia kupungua na unatoa tahadhari kwa wenye cholesterol inakuwaje hapa

  • GigiMaenda says:

   Kwa watu wenye tatizo la cholestérol wanatakiwa kupata ushauri wa daktari kabla ya kula vyakula vyenye cholesterol kiasi fulani. Robo lita ya mtindi full fat ina 12% ya kiasi salama cha Cholestérol cha siku(Recommend daily allowance) kwa watu wengi wenye tatizo hili mtindi hauwaathiri. Lakini kwasababu sifahamu ukubwa wa tatizo wa kila mtu binafsi anayesoma makala hii nimeshauri wenye tatizo wasifate diet hii hadi daktari wao ahakikishe au awaambie wanaruhusiwa kula kiasi gani cha dietary cholesterol kwa siku. Tafiti mpya zinaongezeka ambazo zinasema maziwa ya mgando ingawa yana cholestérol hayaaffect watu wenye tatizo la cholesterol nyingi (https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5867544/ )

COMMENT