DETOX WATER ZINAPUNGUZA UZITO KWELI AU?

Link za tafiti za kisayansi zimeandikwa kwa mfumo wa namba 1-6

Detox water ni maji ya kunywa ambayo hutengeneza kwa kuloweka vipande vya matunda, mboga mboga, majani ya miti shamba au viungo vya kupikia kwa muda wa masaa 1-12 kwenye maji ya uvuguvugu au baridi.

Aina mbalimbali za detox waters zinatengenezwa kwa kutumia mahitaji mbalimbali kama yafuatayo;

 • Limao/ndimu
 • Matango
 • Tangawizi
 • Apples
 • Strawberries
 • Machungwa
 • Majani ya mint au ya Rosemary
 • Pilipili ya unga ya cayenne
 • Mdalasini
Detox water ya limao

Kama wewe umewahi kujaribu kupunguza uzito wa mwili wako basi kuna uwezekano mkubwa sana kwamba umewahi kuambiwa utengeneze detox water hasa ya limao, tangawizi au matango na unywe sana sana kila subuhi kabla ya kula kitu chochote au kabla ya kula mlo wowote wa siku.

MADAI

Detox water huleta faida zifuatazo;

 • Kuyeyusha mafuta mwilini au kupunguza uzito
 • Kutoa sumu mwilini
 • Kusafisha mfumo wa umeng’enyaji chakula
 • Kuongeza nguvu
 • Kukupa mood nzuri

UKWELI

1.Faida hizi zinazosemekana kuletwa na michanganyiko hii ya detox water ndizo faida zinazojulikana za kunywa MAJI kama yalivyo bila kuongezwa kitu chochote. Hii inamaanisha hakuna tofauti kati ya kunywa maji tu au kunywa detox water.

2. Kiasi cha virutubisho kinachotoka kwenye matunda na mboga mboga ni kidogo sana kusababisha faida hizo zinazodaiwa kuletwa na kunywa detox water. Hii ni kwasababu hao matunda na mboga mboga hayasagwi kama juice kwa hiyo virutubisho vingi vinabaki ndani haviingii kwenye maji. Kiuhalisia utapata faida zaidi kwa kula haya matunda kama yalivyo kuliko kuya dilute na maji.

Hii ni kama kusema utengeneze juice halafu uijaze maji ili iwe na ladha karibia na maji. Itabidi unywe lita nyingi sana za maji ili kupata faida ya virutubisho kwa kiasi cha sawa na kunywa juice tu.

3.Kuhusu kutoa sumu mwilini

Hadi leo hakuna tafiti zozote za kisayansi zinazoonesha kuwa binadamu anaweza kunywa au kula kitu ambacho kitasababisha kutoa sumu mwilini au detox.

Njia pekee za kutoa sumu mwilini hufanywa kwa kiasi kikubwa sana na figo, ini na kwa kiasi fulani pia hufanywa na mapafu, ngozi na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.

Na mpaka sasa hakuna tafiti zozote za kisayansi zilizofanywa KWA USAHIHI zinazokubaliana na IMANI hizi za diet au mfumo wa ulaji wa aina yoyote ambao umeonesha kusababisha kutoa sumu au kufanya viungo hivi kutoa sumu kwa ufanisi zaidi. (1)

Ushahidi wa awali unaoonesha baadhi ya mboga mboga kama CORRIANDER (Kotmiri/giligilani), NORI (Mwani = aina ya magugumaji ya baharini yanayoliwa) na OLESTRA (Ni compound inayotengenezwa kutokana na sukari ambayo haina calories na hutumiwa kama mbadala wa mafuta katika kusaidia kupunguza uzito au mafuta mwilini).

Tafiti juu ya vyakula hivi bado hazijakamilika ndiyo maana ushahidi huu ni wa awali.

Kinachosaidia kupungua uzito katika detox water sio vile vitu vinavyowekwa kwenye hayo maji bali ni maji yenyewe. Hakuna tofauti katika faida kwa watu wawili ambao mmoja anakunywa detox water na mwingine anayekunywa maji tupu.

Kazi kubwa ya detox water ni kuongeza ladha kwenye maji ili kusaidia watu wasiopenda kunywa maji kwa wingi waweze kufurahia kunywa maji.

Kunywa maji mengi kunasaidia sana kupunguza uzito kwa njia zifuatazo.

 • Maji hujaza tumbo hivyo kukufanya ujisikie umeshiba.
 • Hupunguza njaa na hamu ya kula. ( 2, 3 )
 • Huongeza uwezo wa mwili wako kutumia sukari, glycogen au mafuta kutengeneza nguvu hivyo kukufanya uchome calories nyingi na kusaidia kupunguza uzito.( 4 , 5 )
 • Huimarisha mfumo wa mmeng’enyo wa chakula hivyo kusaidia kupata choo ipasavyo. Kutokunywa maji mara kwa mara husababisha choo ngumu(constipation) ambayo inaweza kupelekea tumbo kuonekana limejaa (Bloating) ( 6, 7 )

KWA UFUPI NI KWAMBA

 • Watu wengi wanatumia detox water kwasababu wamesikia kuwa zinatumika kuyeyusha mafuta mwilini na kupunguza tumbo. Faida nyingi zinazohusishwa na unywaji wa detox water haziendani na misingi ya kisayansi na baadhi tu zina ukweli . Faida ya kupungua uzito hutokana na kunywa maji kiasi kingi na siyo vitu vilivyowekwa kwenye hayo maji.

Kwa hiyo usijilazimishe kuongeza vitu vyovyote kwenye maji kama limao, tangawizi, matango au majani ya yoyote kama tayari hauna tatizo la kunywa maji kwa wingi.

Kama wewe ni mmoja wa watu ambao hawawezi kunywa maji kwa kiasi kinachotakiwa basi utafaidika kutumia detox water kwasababu kazi pekee ya detox water ni kuongeza kidogo ladha ya maji ili kukusaidia upende kuyanywa.

SOMA ZAIDI

You may also like...

COMMENT